Wakaazi wa Narok Mashariki Wamuomba Kamishna Kusaidia Kutatua Mzozo Unaolemaza Maendeleo

Narok: Wakaazi wa kijiji cha Olesimu katika eneo la Oletukat, Narok Mashariki sasa wanamtaka kaunti kamishna wa Narok, Bwana Kipkech Lotiatia kuingilia kati mzozo unaotokota katika kanisa la kiadventista (SDA) unaosababisha uhasama miongoni mwa waumini.

According to Kenya News Agency, baadhi ya viongozi wa kidini wa kanisa hili wanapinga mradi wa maji unaolenga kuwanufaisha takriban familia 1,000 kutoka eneo hili kwa manufaa yao ya kibinafsi. Akizungumza na waandishi wa habari, Julius Nchosoi alisema wamefanya juhudi zote kwenda kuripoti hadi kwa chifu wa eneo hilo lakini amesalia kimya licha ya chifu huyo kuelewa vyema kuwa wenye ranchi ya kikundi cha Oletukat walitoa kipande cha ardhi cha ekari 50 kwa kanisa hili wakati ambapo alikuwa mweka hazina wa kikundi hiki.

Kundi pinzani linaloongozwa na mchungaji Stanley Nkere lilifika wakati wa ibada ya Jumamosi na kushambulia waumini kanisani. Baadhi yao walipata majeraha makali kiasi cha kukimbizwa hospitalini kwa matibabu. Mchungaji Benson Nchosoi alisema kwamba hawako tayari kushirikiana na wale wanaopinga miradi itakayowanufaisha wakaazi wa eneo hili ambao wamesumbuka kupata bidhaa hii muhimu wanayoipata takriban kilomita arobaini kutoka wanapoishi.

Mchungaji Nchosoi aliweka bayana kwamba wakati kanisa hili lilipokabidhiwa shamba hili, kuliwekwa makubaliano ya kwamba wataweka miradi itakayowasaidia wakaazi hapa na chifu alikuwa shahidi wakati mkataba huu ulipowekwa. Nchosoi aliendelea kusema kuwa mradi wa shule ulikamilika, ule wa ujenzi wa hospitali uko karibu kuisha na wakaazi waanze kupata huduma za afya lakini ule wa maji ambapo ulianza kushughulikiwa Ijumaa iliyopita umezua vurugu akiwanyoshea kidole kundi pinzani kwa kuwa mawakala wa kupinga maendeleo kwa sababu wanazozifahamu wao wenyewe.

Sasa, wakaazi wameapa kutowakaribisha wale wasiotaka maendeleo kwa sababu wanahitaji huduma ya maji haraka iwezekanavyo ili waendelee na maisha yao ya kawaida.